Baraza la vijana CHADEMA (BAVICHA) limewataka watanzania wote kwa ujumla hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza siku ya kesh...
Baraza la vijana CHADEMA (BAVICHA) limewataka watanzania wote kwa
ujumla hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza siku ya kesho
(Jumapili) katika maombi ya Tundu Lissu kwa madai wamekamilisha taratibu
zote za kisheria juu ya jambo hilo.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Mkuu (BAVICHA) Taifa, Julius Mwita kupitia
ukurasa wao maalum wa Facebook wa chama hicho baada ya siku ya jana
Kamishna Kanda maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa kuzuia
kufanyika kwa maombi hayo.
"Kupitia kamati ya
maandalizi, BAVICHA inapenda kuwaambia Watanzania wote ambao watapenda
kuhudhuria maombi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kuwa
maandalizi yote muhimu yameshafanyika kwa ajili ya kuhakikisha shughuli
hiyo ya kiimani inafanyika kama ilivyopangwa", amesema Mwita.
Julius Mwita aliendelea kwa kusema mpaka
sasa wameshafuata taratibu zote za kisheria ambazo zimewaelekeza kutoa
taarifa kwa mamlaka za kiserikali hususani Jeshi la Polisi
"Hadi sasa jeshi hilo
halijatuandikia barua ya kutuita ili kujadiliana nao kuhusu kufanikisha
shughuli hiyo, tunaamini kuwa hawana pingamizi lolote la kiutaratibu
kama ambavyo sheria inaelekeza. Tumefuatilia kwa kina kuhusu kauli za
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambazo
zimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo ikidhaniwa kuwa amezuia
shughuli hiyo ya maombi, na tumebaini kuwa ZPC Mambosasa hakueleweka
vyema", amesema Mwita.
Pamoja na hayo, Mwita ameendelea kwa kusema
"Tumejiridhisha tena kuwa taarifa tuliyopeleka kwa jeshi la polisi kama
sheria inavyoelekeza, tukiwataarifu kuhusu maombi hayo, haikutaja wala
kuzungumzia maandamano bali watu wa dini mbalimbali zilizopo nchini
wanaoguswa na tukio la Lissu na maumivu anayopitia hospitalini,
watakutana na kuomba sala au dua ili Mwenyezi Mungu afanye uponyaji kwa
mgonjwa wetu", amesisitiza Mwita.