Dodoma. Siku chache baada ya ofisa wa Ikulu, Frank Lyimo kufariki dunia baada ya kuumwa na nyuki, Manispaa ya Dodoma imebaini maeneo manne y...
Dodoma. Siku chache baada ya ofisa wa Ikulu, Frank Lyimo kufariki dunia baada ya kuumwa na nyuki, Manispaa ya Dodoma imebaini maeneo manne yenye makundi ya nyuki ambayo ni hatari kwa binadamu.
Maeneo yaliyobainika kuwa na makundi ya nyuki ni Zahanati ya Makole, Dodoma Makulu, Kisasa na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Ofisa Nyuki wa Manispaa ya Dodoma, Vedastus Milinga alisema baada ya tukio la Lyimo kung’atwa na nyuki wakati akipita katika nyumba ya kulala wageni ya Formula One eneo la Makole mjini hapa, wamepokea taarifa za uwapo wa nyuki kwenye maeneo mengine.
“Sasa hivi nyuki wapo wengi mtaani kwa sababu wanatafuta mizinga. Hivyo wakazi wa mji huu wanatakiwa kutupatia taarifa wanapoona makundi ya nyuki ili tuwaondoe,” alisema Milinga.
Akizungumzia suala hilo Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kati, Mathew Kiondo alisema baada ya kubaini uwapo wa nyuki wamemwagiza ofisa nyuki wa manispaa ya Dodoma kupeleka bajeti kwa ajili ya kuwaondoa.
Alisema tangu mwaka huu uanze kumekuwa na matukio matatu ya watu kufa kwa kuumwa na nyuki katika maeneo ya Hombolo, Makutopora na Makole.
“Tumeamua kuanza kutoa elimu kwa wananchi wajue umuhimu wa kutoa taarifa na kutoa huduma ya kwanza wakati
mtu anapoumwa na nyuki,” alisema.
Alifafanua kuwa watapitisha gari la matangazo na vipindi vya redio kutoa elimu hiyo.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Mwenyekiti wa Makole, Anne Ngaya kueleza kudaiwa gharama za kuondoa nyuki katika eneo lake, Kiondo alisema kazi ya TFS ni kutoa ushauri kwa ufugaji wa nyuki. “Hatuwezi kufahamu kuhusu uwapo wa nyuki bila kupata taarifa kutoka kwa wananchi au viongozi ambalo ni jukumu lao. Na hii operesheni ya kuondoa nyuki ina gharama zake ambazo ni lazima mtu atatakiwa kutoa kwa ajili ya kununulia dawa,” alisema.
Kiondo alisema majibu aliyoyapata Anne kuwa kuna gharama za kugharamia kazi hiyo ni sahihi kwa kuwa ofisi hiyo haipangi bajeti kwa ajili ya kuteketeza nyuki.