Rais wa sasa wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS, Tundu Antiphas Mughway Lissu amependekezwa kutetea Urais wa chama hicho katika u...
Rais wa sasa wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS, Tundu Antiphas Mughway Lissu amependekezwa kutetea Urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao jijini Arusha. Lissu ambaye amekuwa kwenye matibabu kwa muda sasa akitibu majeraha ya shambulio la risasi, alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa TLS mwaka jana.
Taarifa za kuaminika kutoka TLS zinadokeza kuwa Lissu anapigiwa chapuo na Mawakili wengi kwa mambo mawili:
Mosi, ni kutokana na kutekeleza mambo mengi kati ya yale aliyoyaahidi wakati akiomba kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS. Mambo hayo ni pamoja na kuifanya TLS kurudi kwenye misingi na majukumu yake pamoja na kusimamia ujenzi wa Jengo la TLS uliosuasua kwa muda mrefu.
Mambo mengine aliyoyaahidi na kuyatekeleza ndani ya mwaka mmoja wa Urais wake ni kupunguza au kuweka uwiano wa michango ya Mawakili huku Mawakili wakongwe wakitofautishwa na Mawakili wachanga. Tayari michango inatofautiana kati ya Wakili na Wakili kwa kuzingatia ukongwe. Tena, michango mingine imefanywa kuwa ni ya hiari.
Pamoja na kutokuwepo ofisini kwa muda mrefu, Lissu anatajwa kama mgombea (akipitishwa na Kamati ya Kuratibu Uchaguzi wa TLS) mwenye nguvu na asiyehitaji nguvu kubwa kujieleza au kuelezwa. Changamoto pekee itakuwa ni katika uwepo wake uchaguzini ingawa Mawakili wengi wameapa kumpigia kampeni na kumchagua kwa kishindo kikubwa hata asipokuwepo.
Sababu ya pili ya Lissu kupigiwa upatu ni kuwa Lissu ni mmoja wa Mawakili wenye uthubutu na anayeweza kuwasilisha maoni, mapendekezo na mawazo ya TLS kwa mamlaka yoyote bila woga, mawaa wala tatizo. Lissu pia ameiva katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza ambazo ndizo hasa hutumika katika shughuli za kila siku za TLS.
chanzo........Jamiiforums