Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), imevipika marufuku takribani vyuo 163 vilivyopo nchini Tanzania kuacha kuwafanyia udahili w...
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), imevipika
marufuku takribani vyuo 163 vilivyopo nchini Tanzania kuacha kuwafanyia
udahili wa masomo wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu kwa
mwaka 2018 kutokana na kutokidhi vigezo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Udahili Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi, Twaha Twaha leo (Machi 23, 2018) wakati
walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na
kusema baraza linawataka waombaji wa nafasi za mafunzo kwa ngazi za
Astashahada na Stashahada kwa muhula wa masomo wa Machi/Aprili, 2018
kuomba kwenye vyuo vilivyokidhi ubora ambavyo vimeorodheshwa kwenye
tovuti ya baraza na sio vinginevyo.
"Baraza lilifanya uhakiki 'academic audit' kwenye vyuo
vyote ambavyo vimesajiliwa na baraza ili kuweza kujiridhisha kuona
kwamba vina sifa na mambo mbalimbali ambayo yanahusika na utoaji wa
taaluma. Katika uhakiki huo, Baraza lilibaini kuwa baadhi ya vyuo
vilikidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa taratibu za Baraza. Hata
hivyo, baadhi ya vyuo vilibainika kuwa na changamoto mbalimbali
zinazoweza kuathiri ubora wa elimu na mafunzo yanayotolewa", amesema
Twaha.
Pamoja na hayo, Twaha ameendelea kwa kusema "kufuatia zoezi
hilo vyuo vyote vilivyobainika kuwa na mapungufu vilitaarifiwa na
kutakiwa kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa kabla ya kuendelea na
udahili wa wanafunzi kwa mwaka mpya wa masomo 2018/2019".
Kwa upande mwingine, Twaha amesema kuwa udahili wa muhula
wa Machi/Aprili, 2018 hauhusishi programu zote za kada ya Afya na
Ualimu.