Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na Uvumi katika Mitandao ya Kijamii kuwa Serikali imeamua kushusha Mishahara ya Madaktari kwa asi...
Katika
siku za hivi karibuni kumekuwa na Uvumi katika Mitandao ya Kijamii kuwa
Serikali imeamua kushusha Mishahara ya Madaktari kwa asilimia 30% ili
kuendana na dhana ya Hapa kazi tu na kuwa Serikali imekusudia kufuta
malipo ya Posho za Wataalamu wa Afya walio katika Mafunzo kwa Vitendo
.Ufafanuzi kwa Umma wa Watanzania na Watumishi wa Sekta ya Afya ni kuwa
taarifa hizo siyo za kweli.
Taarifa
aliyoitoa Katibu Mkuu (Afya) alipokuwa anaongea na Watumishi wa
Hospitali ya Bugando ililenga kutoa ufafanuzi kwa Watumishi wa
Hospitali hiyo kuhusu kufutwa kwa kibali cha Msajili wa Hazina
kilichowawezesha watumishi wa Hospitali hiyo kulipwa Mishahara ya
Taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina tangu mwaka 2012.
Uamuzi
huo wa Msajili wa Hazina unatokana na ukweli kwamba Hospitali ya
Bugando siyo Shirika la Umma na hivyo wanastahili kulipwa mishahara sawa
na watumishi wengine wa Serikali Kuu kwa kuzingatia makubaliano
yaliyopo kati ya Serikali na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambao
ndio wamiliki wa Hospitali ya Bugando.
Aidha,
ieleweke kuwa mishahara ya Watumishi wa Sekta ya Afya haizingatii ngazi
ya Vituo vya kutolea huduma kama vile Zahanati, Kituo cha Afya,
Hospitali, au Hospitali za Rufaa bali huzingatia uzito wa kazi na
majukumu ya kada husika. Hivyo, mshahara wa Daktari wa Hospitali ya
Wilaya ni sawa na ule wa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa na Hospitali
ya Rufaa ya Kanda.
Kutokana
na maelezo haya, uamuzi huo wa Msajili wa Hazina utaihusu Hospitali ya
Bugando pekee na siyo Hospitali zote za Kanda kwa kuwa dosari hiyo
haikutokea katika Hospitali nyingine za Kanda.
Kuhusu
ajira mpya kwa mwaka 2015/2016 ufafanuzi ulitolewa na Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hakutakuwa na ajira mpya hadi
hapo Zoezi la Uhakiki wa Watumishi Serikalini litakapokamilika. Hivyo,
vibali vya ajira vilivyokuwa vimetolewa vimefutwa hadi hapo
itakapotamkwa vinginevyo.
Kadhalika,
kumekuwa na Uvumi kuwa Serikali inakusudia kufuta posho ya ‘Interns'
kuanzia mwaka huu wa fedha. Taarifa hii pia siyo sahihi kwa kuwa hakuna
chombo chochote cha Serikali ambacho kimetoa maamuzi hayo.
Wizara
inasisitiza kuwa maamuzi ya Serikali hutolewa na Mamlaka husika kwa
nyaraka. Hivyo, watumishi wa Sekta ya Afya na wananchi kwa ujumla
wanaaswa kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka za Serikali kuhusu
Masuala yanayowahusu ambayo mara nyingi hutolewa kwa nyaraka badala ya
Mitandao ya kijamii,
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Afya
14 Julai, 2016