Watu watatu wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kupelekwa hospitali ya Alr...
Watu watatu wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa vikosi vya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kupelekwa hospitali ya Alrahma
kwa matibabu.
Majeruhi hao ni Yussuf Ali Juma (23), Ali Shaame
Ibrahim (18) na Salim Masoud Bakar (18), wakazi wa Tomondo Wilaya ya
Magharibi Unguja.
Kabla ya watu hao kujeruhiwa, milio ya risasi
ilitawala jana majira ya saa 8:30 mchana katika mitaa ya Tomondo,
Mwanakwerekwe na Kilimani, hivyo kuzua taharuki miongoni wakazi wa mitaa
hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa waliyaona magari ya vikosi
hivyo yakiendeshwa kwa mwendo kasi kuzunguka maeneo hayo huku yakiwa na
askari wakifyatua risasi.
“Mimi kwa sasa nipo hapa Kilimani na
hivi punde tu risasi tumezisikia kutokea upande huu wa Mwanakwerekwe na
Jang’ombe na ghafla naona watu wanakimbizwa kuletwa hapa Alrahma”
alisema Rashid Said (54), mkazi wa Migombani ambaye ni dereva teksi.
Majeruhi
Ibrahim alisema: “Walikuja wale mazombi, wengine walifunika uso
waliwafungua ng’ombe wetu na kutaka kuwachukua, kwanza wakapiga risasi
juu, tulipoona wanawapakiza katika magari lao tukasogea ndipo wakatupiga
risasi.”
Bakari Juma (35), mkazi wa Msheleshelini alisema:
“Tunasikia hawa jamaa wanataka wauze kitoweo cha nyama siku za sikukuu
peke yao, lakini miye nasema sawa wafanye hivyo, ila si kwa ng’ombe wa
kupora.”
Baadhi ya wananchi walidai kuwa mifugo hiyo wakiwamo ng’ombe wa maziwa ni mali yao.
Mmoja
wa wafugaji hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Omar alisema: “Sisi
tunafuga ng’ombe hawa kama mnavyoyaona mabanda yetu yapo si miaka kumi
wala ishirini ni tangu zamani wakati huo Tomondo ni pori tupu na mpaka
sasa mifugo yetu haizururi wala haimkeri mtu yeyote.”
Licha ya
askari kudaiwa kufika eneo la tukio na katika hospitali walikolazwa
majeruhi hao, hali ya usalama ilionekana kuyumba pale makundi ya watu
yalipohamasika kusogelea maeneo hayo.
Waliofika katika hospitali
hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano kwa Umma wa Chama
cha Wananchi (CUF), Salim Abdalla Bimani.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuahidi kufuatilia zaidi ili kubaini chanzo chake.
Hata hivyo, alisema polisi waliingilia kati na kwenda katika maeneo hayo kurejesha hali ya usalama.
“Sijapata
kwa ukamilifu kilichotokea, lakini ni kweli hawa vikosi wanaendesha
operesheni ya kukamata ng’ombe wanaozurura mitaani, wamekwenda huko na
kukatokea kukwaruzana baada ya kuwepo vijana ambao hawataki kuondoa
ng’ombe, nimepeleka askari kutuliza hali na sasa hali imekuwa ya amani”,
alisema Kamanda Mkadam.