Ujumbe wa mabalozi , na maofisa wa ngazi za juu wa balozi za Umoja wa nchi za Ulaya (EU) pamoja na Canada umefanya ziara ya kikazi kati...
Ujumbe wa mabalozi , na maofisa wa ngazi za juu wa balozi za Umoja wa nchi za Ulaya (EU) pamoja na Canada umefanya ziara ya kikazi katika Baraza la Habari Tanzania Jijini Dar es Salaam ambapo ulijadili hali
ya vyombo vya habari nchini Tanzania ikiwamo kufungiwa kwa magazeti mawili ya Kiswahili – Mwananchi na Mtanzania.
Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Umoja wa Ulaya , Filiberto C. Sebbregondi.
Masuala yaliyozungumzwa katika mkutano huo uliofanyika katika ofisi za MCT Oktoba 7, 2013 ni pamoja na hali ya sheria za vyombo vya habari nchini Tanzania na kuona kama zinakwaza uhuru wa habari, weledi kwenye vyombo vya habari na Baraza linafanya nini kuboresha uandishi wa habari.
Mkutano huo pia ulijadili kuhusu hali ya vitisho dhidi ya haki za kitaaluma za waandishi wa habari ikiwemo hata mauaji yakitolewa mfano wa mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi mwaka jana.
Kwa jumla mabalozi hao wanaunga mkono uhuru wa habari na wamesisitiza kuwa uhuru huo ni nguzo muhimu ya demokrasia.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, aliwaambia mabalozi hao kuwa , ” Hatusemi kuwa hakuna makosa katika vyombo vya habari. Lakini tunasema makosa haya yasichukuliwe kama ni uhalifu kwani kuna njia nyingi ya kuyashughulikia..
“ Inasikitisha kwamba wakati tunapata sifa nzuri kwamba serikali yetu inakuza uwazi na kwamba Rais wetu ana dhamira kubwa ya kuendesha serikali kwa uwazi , ghafla serikali inafanya maamuzi kinyume na sifa inayojijengea”, alisema.
Katika taarifa iliyotolewa na Umoja huo wa Ulaya kufuatia kufungiwa kwa magazeti hayo mawili, umeitaka serikali kuchukua hatua za kudumisha uhuru wa habari na kukuza haki ya kupata habari.
Umoja huo umeeleza katika taarifa hiyo kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuendeleza majadiliano kama hatua ya msingi ya kutatua tofauti.
Mabalozi wengine waliokuwemo kwenye ujumbe huo ni Olivier Chave wa Uswsi, Lennarth Hjelmaker wa Sweden, Johnny Flento wa Demanrk, Sinikka Antila wa Finland, Luis Guesta wa Hispania, Koen Adam wa Ubelgiji na Jaap Frederiks wa Uholanzi.
Wengine ni Balozi wa Canada Patricia McCullagh, Tom Vens mwanadiplomasia wa EU , Claude Blevin wa Ubalozi wa Ufaransa, Maire Matthews wa Ubalozi wa Ireland, Lise Stensrud wa Norway na Ofisa wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) Marcelina Biro.