WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia machimbo ya madini ya dhahabu ya Ifumile Kijiji cha Isumamilomo Wilaya...
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia
machimbo ya madini ya dhahabu ya Ifumile Kijiji cha Isumamilomo
Wilaya ya Mpanda na kumuua mchimbaji mmoja kwa kumpiga risasi.
Watu hao wanadaiwa kumpiga risasi ya tumboni kwa kutumia bunduki aina ya AK 47 na kujeruhi wengine watatu.
Pia wanadaiwa kupora dhahabu yenye uzito wa zaidi ya
gramu 650, fedha taslimu Sh. milioni 1.5 na mashine mbili za
kutafutia dhahabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alisema jana kuwa wandishi tukio hilo lilitokea juzi usiku.
Alisema siku ya tukio majambazi hao ambao
waliokuwa watatu walifika katika machimbo ya Ifumile wakiwa
wamejifunika sura zao kininja na kuwashambulia kwa risasi
wachimbaji na wanunuzi wa dhahabu.
Alisema waliwajeruhi wachimbaji watatu sehemu mbalimbali
za miili yao huku baadhi wakinusurika baada ya kukimbilia kwenye
vichaka.
Kamanda Nyanda alimtaja aliyeuawa ni Sita Kalyalya
(34), mkazi wa Bariadi Shiyanga ambae alipingwa risasi ya
tumboni na mkononi na alifariki dunia muda mfupi baada ya
kufikishwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda akiendelea
kupatiwa matibabu.
Aliwataja waliojeruhiwa ni Joseph Panya (34) ambaye
amejeruhiwa kwenye bega la kushoto na mguu wa kulia, Mrisho
Rashid (21 ) aliyejeruhiwa mguuni na mkono wa kulia na Masunju
Mgulu (28) aliyejeruhiwa mguu na mkono wa kushoto.
Kamanda Nyanda alisema majambazi hao baada ya
kuwajeruhi wachimbaji walipora fedha hizo, dhahabu na mashine za
kutafutia dhahabu kisha kutokomea.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya tukio hilo polisi
walifika eneo la tukio na kuokota risasi 24 na maganda saba ya
risasi zilizotumika za bunduki iliyotumika kwenye tukio hilo.
Nyanda, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka majambazi hao
na alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa
kutoa taarifa zitakazowawezesha kuwatia nguvuni.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya
Mpanda, Dk. Jaffari Masanja, alisema marehemu Kalyalya alifariki
muda mfupi baada ya kutolewa kwenye chumba cha upasuaji.
Alisema majeruhi Panya na Rashid walikuwa wamelazwa
katika wodi namba moja wamepewa rufani na wamesafirishwa kwenda
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu
zaidi baada ya hali zao kuwa mbaya, Alisema Mgulu amebaki
hospitali huku hali hiyo yake ikiendelea kuimarika.



