WAHITIMU wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Ruhuwiko katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kujiepusha kufanya vitendo ...
WAHITIMU wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Ruhuwiko katika
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kujiepusha kufanya vitendo
vya udanganyifu kwenye mitihani.
Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani humo,
Angelo Maskini alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu
na wazazi wakati wa mahafali ya 11 ya kidato cha sita katika shule hiyo,
inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Brigedi ya Tembo.
Kwa mujibu wa Maskini, muda uliobaki kabla ya kufanya mitihani yao ni
mdogo, kwa hiyo ni vema kuutumia kwa ajili ya kujikumbusha mambo ya
msingi waliyofundishwa na walimu wao badala ya kuwa na mawazo mabaya ya
kutamani kushiriki katika vitendo ambavyo vitawavunjia heshima na
kukatisha ndoto zao.
Maskini alipongeza wahitimu hao kwa kufanikiwa kutimiza nusu ya ndoto
walizonazo. Aliwataka kutoridhika na kiwango cha elimu walichonacho
bali wawe na fikra na malengo makubwa ya kuendelea na elimu ya chuo
kikuu ambayo inahitajika sana katika ulimwengu wa sasa.
Aidha, alikumbusha wazazi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kutoa
ada na mahitaji mengine yanayohitajika kwa ajili ya watoto wao. “Wazazi
wenzangu ni lazima sasa tubadilike tuache kutumia kiasi kikubwa cha
fedha katika anasa, tujitahidi kutoa michango ya shule kwa ajili ya
watoto wetu kwa muda muafaka ili wapate muda mwingi wa kujisomea,”
alisema Maskini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Brigedi ya 401 KV Tembo, Brigedi
Kanali Iddi Nkambi amewataka wahitimu hao kwenda kuishi maisha ya
kuiogopa zaidi dunia kama walivyokuwa wakiishi wakati wakiwa shuleni.
Nkambi ambaye pia ni Mkuu wa mafunzo na utendaji kivita, aliwataka
vijana hao kuwa raia wema na kulinda nchi yao pamoja na kujiepusha
kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na upendo uliopo tangu uhuru.
Mkuu wa shule hiyo, Meja Paul Rugwaguza alisema, vijana hao
walipokuwa shuleni walilelewa kwa nidhamu na kuandaliwa kuwa watu wema
katika jamii. Rugwaguza alisema, shule hiyo ni kati ya shule bora ambazo
zinafanya vizuri katika matokeo ya mitihani mbalimbali ya kujipima
uwezo na hata ile ya kitaifa.