MKUU wa Shule ya Sekondari Kakonko wilayani Kakonko mkoani Kigoma,Peter Rubonya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba ofisini k...
MKUU wa Shule ya Sekondari Kakonko wilayani Kakonko mkoani
Kigoma,Peter Rubonya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba
ofisini kwake mapema leo asubuhi.
Akielezea tukio hilo,Mwalim wa zamu wa shule hiyo Isaac
Japhet amesema yeye alifika shuleni hapo saa 12:30 asubuhi ili
kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha nne masomo ya ziada baada ya
kufunga shule wiki iliyopita na baada ya kufika aligundua kuwa hana
chaki ambapo mkuu huyo wa shule alimpatia chaki mlinzi ili awape
wananfunzi.
Amesema baada ya muda,Mratibu elimu kata pamoja na mmoja wa
wazazi walifika ofisini hapo wakiwa na shida na mkuu wa shule na baada
ya kuelezwa yupo ndani ofisini lakini baada ya kugonga mlango hawakuweza
kujibiwa na ndipo wakaamua kufungua mlango na kukuta mwili wa marehemu
ukining’inia dalini.
Mwalim Isaac amesema Mwalimu aliyejinyonga alikuwa
akifundisha masomo ya Kemia na Fizikia shuleni hapo hawakuwahi kusikia
mgogoro wowote wa kifamilia au kijamii, na mkewe ambaye ni mkufunzi
katika Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM),alifika nyumbani kwake juzi akitokea
Dodoma.
Kwa upande wa Mlinzi wa Shule hiyo Kajolo Kajabojabo
amesema alikutana na Mkuu wa shule mapema asubuhi akiingia ofisini na
kumuomba chaki ambazo alipewa na kuziwasilisha kwa walimu.
"Nilimuona kabisa tukasalimiana, nikamuuliza kama anaweza
kuwa na chaki, akaingia ofisini akanipatia boksi moja la
chaki.Nikachukua na kisha nikampelekea mwalim aliyehizihitaji, alikuwa
kwenye hali nzuri tu, lakini baada ya muda ndo tukio hilo
likatokea,"amesema Kajoro.
Akizungumza baada ya kufika shuleni hapo Mkuu wa Wilaya ya
Kakonko Kanali Hosea Ndagala amesema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo kujua sababu ikiwa marehemu aliacha ujumbe wowote au laa.
"Hatujajua sababu lakini ni muhimu jamii ikajenga utamaduni
wa kueleza matatizo ya ndani yanayoyasibu.Hiyo inasaidia kupunguza
msongo wa mawazo na kuepusha madhara kama haya,"amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Martin Otieno amesema
baada ya kupekuliwa kwa mwili wa marehemu walikuta karatasi imeandikwa
ujumbe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko Lusubiro Mwakabibi
asipodhibitiwa ataua wengi.