Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamsaka mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mwita Marwa (30) kwa tuh...
Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamsaka mwanafunzi wa
mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mwita Marwa (30)
kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga mpenzi wake Kibua Adam (39) baada ya
kutokea kutokuelewana kati yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema
tukio hilo lilitokea Januari 22 mwaka huu katika eneo la Modeco Manispaa
ya Morogoro ambapo mwanafunzi huyo alitoweka baada ya tukio hilo.
Amesema siku ya tukio mwanafunzi huyo na mpenzi wake ambaye
ni mhudumu wa baa walichukua chumba katika nyumba ya kulala wageni
ijulikanayo kama Aluta ambapo walilala lakini baadaye mwili wa marehemu
ulikutwa chumbani.
“Dada huyu mkazi wa Kihonda alikutwa ameachwa chumbani
akiwa ameshafariki na baada ya uchunguzi ilionekana kwamba marehemu
alinyongwa shingo kabla ya kifo chake,” amesema Kamanda Matei.
Hata hivyo, kamanda huyo amesema baada ya tukio hilo
mtuhumiwa alimwandikia ujumbe wa simu dada wa marehemu aitwaye Happiness
Adamu ujumbe akisema kwamba tayari marehemu keshatangulia na yeye
mtuhumiwa atafuata.
“Nasikitika sana hamtatuona hapa duniani Mwita na Kibua,
mimi ninayeandika meseji hii ni Mwita, nikimaliza nakunywa sumu au
vidonge nife na mimi nimechoka na dunia na Kibua yeye keshatangulia,
njooni hapa Aluta Bar mtutoe chumbani tulipolala,” ulisomeka ujumbe huo.
Hata hivyo, watu wa karibu wa marehemu ambao hawakutaka
kutaja majina yao walisema marehemu alikuwa na mpenzi mwingine kabla ya
Mwita na walipokorofishana ndipo alipoamua kuwa na Mwita lakini siku
chache kabla ya tukio alimwambia Mwita kwamba mpenzi wake wa awali
amejirekebisha hivyo anataka kurejeana naye jambo ambalo mtuhumiwa
alikuwa analipinga.
Kamanda Matei amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika
Hospitali ya Mkoa ya Morogoro na jeshi hilo bado linaendelea na
jitihada za kumsaka mtuhumiwa.