WATU watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa vyuo vikuu vilivyoko jijini Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mk...
WATU
watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa vyuo vikuu vilivyoko jijini Dar es
Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Wanafunzi
hao ni wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Hussein Mustafa (26) na wa Chuo Kikuu
Huria (OUT), Haruna Nkuye (24) ambao wanashitakiwa pamoja na fundi
makenika Rajabu Ally (41) wote wakazi wa Dar es Salaam.
Washitakiwa
hao wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo kwenye tukio la ujambazi katika
Benki ya CRDB eneo la Chanika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, walisomewa
mashitaka na Wakili wa Serikali Jackson Chidunda mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu Huruma Shahidi.
Akisoma
hati ya mashitaka, Chidunda alidai Desemba 8, mwaka jana katika eneo la
Chanika, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, washitakiwa walimuua Ramadhani
Halili, Shan Rajabu na Thomas Otemu.
Hakimu
Shahidi alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu mashitaka kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama
Kuu.
Upande
wa jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba
tarehe nyingine ya kutajwa ili wamuunganishe mshtakiwa Mohamed Ungando
ambaye jana hakuwepo mahakamani.
Awali,
mshitakiwa Mustafa aliiomba mahakama imsaidie apate matibabu kwa kuwa
viungo vinamuuma kutokana na adhabu alizopewa akiwa mahabusu.
Hakimu
Shahidi alisema gerezani kuna utaratibu wa matibabu, kama hatatibiwa
kesi itakapotajwa tena aijulishe mahakama. Kesi hiyo imeahirishwa hadi
Julai 14, mwaka huu.