Mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoani hapa, Daudi Mwangosi, Pacificus Simoni ametoa ushahidi wake ...
Mtuhumiwa
wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoani hapa,
Daudi Mwangosi, Pacificus Simoni ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama
na kuieleza kuwa alilazimishwa kusaini ungamo mbele ya mlinzi wa amani
bila kujua nini kilichoandikwa.
Alidai
kuwa baada ya kutoka kuhojiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na
Ofisa wa Makosa ya Jinai ya Mkoa (RCO), akifananishwa na picha ya gazeti
la Mwananchi la Septemba 3, 2012 alipokana siyo yeye, alipelekwa kwenda
kufanya ungamo kwa mlinzi wa amani, Frola Mhelela ambaye alikuwa
shahidi namba tatu.
Alidai
wakati anakwenda kwa mlinzi wa amani alisindikizwa na Staff Sajent
Erick, ambaye alikuwa ameshika bahasha na kumkabidhi kwa mlinzi huyo.
Mtuhumiwa
huyo alidai mlinzi huyo alitoa karatasi na kuisoma kisha baadaye
alimuambia aisaini, naye bila kuhoji alisaini ile karatasi kwa sababu
ilitoka kwa kiongozi wake ambaye ni RCO, Nyegesa Wankyo.
Katika
kesi hiyo wakili wa utetezi, Rwezaura Kaijage aliiomba Mahakama kwamba
mawakili wa upande wa Jamhuri wataleta majumuisho ya mwisho leo.
Hata
hivyo, upande wa jamhuri ambao uliongozwa na wakili Sunday Hyera,
ulisema hawana pingamizi lolote juu ya upande wa utetezi baada ya kukaa
na kukubalina kwa pande zote mbili saa nane mchana watawasilisha
majumuisho hayo.
Jaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk Paulo Kihwelo alisema Mahakama
imekubali ombi la wakili wa utetezi kuleta majumuisho, huku Juni 27
wakisikiliza maoni ya wazee wa baraza kwa ajili ya kupanga hukumu.