Mchungaji na mke mpya wakiwa kanisani. HII ni aibu ya baba mchungaji! Mchungaji wa Kanisa la Elgibbon Ministry l ililopo Songwe mkoani...
Mchungaji na mke mpya wakiwa kanisani.
HII ni aibu ya baba mchungaji! Mchungaji waKanisa la Elgibbon Ministry lililopo
Songwe mkoani Mbeya, Imani Kalinga amejikuta akipata aibu ya aina yake
baada ya kufumwa laivu na mkewe akifunga ndoa na mwanamke mwingine
mrembo (kifaa) aliyefahamika kwa jina la Bupe Kajigili.
NI JUMAMOSI ILIYOPITA
Tukio hilo lililozua taharuki kwa waumini waliokuwa
wakifuatilia ibada hiyo ya ndoa, lilitokea Jumamosi iliyopita ambapo
mchungaji huyo alimuacha mkewe Mbeya na kuja jijini Dar kufunga ndoa na
mwanamke huyo katika kanisa moja lililopo Kibamba Kibwegele.

Mchungaji na mkewe wa zamani.
TAARIFA ZA AWALI
Awali, ilidaiwa kuwa mchungaji Imani alikuwa na mgogoro wa
ndoa na mkewe Elizabeth Jeremiah ambapo kesi yao ilitakiwa kutolewa
uamuzi na Mahakama ya Mwanzo ya Mbalizi, Machi 5 mwaka huu ambapo kabla
ya tarehe hiyo, mchungaji huyo akaamua kutaka kuoa bila kumtaarifu
mkewe.
MKE ATONYWA
Wakati mchungaji huyo akiwa kwenye mipango yake ya siri,
wapambe walimtonya mkewe kuwa mumewe alikuwa Dar kwa ajili ya kufunga
ndoa na mwanamke mwingine.
Taarifa hizo zilimshtua mwanamke huyo ambaye alifunga
safari toka Songwe mpaka Dar akiwa ‘jeshi’ lake na kufanikiwa kumkuta
mumewe akiwa madhabahuni na Bupe huku vigelegele na wimbo wa
‘wanameremeta’ ukiwa umetawala kanisani hapo.

MKE AVAMIA
Baada ya kushuhudia hayo, Elizabeth alivamia madhabahuni na
karatasi za mahakamani na vielelezo lukuki kuhusu ndoa yao ambapo
alimuonesha Mchungaji Steven Jungwa aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo.
Mchungaji Jungwa ambaye anadaiwa kumfahamu vizuri mchungaji
mwenzake Imani na mkewe Elizabeth, alianza kurushiwa lawama na mwanamke
huyo aliyekuwa akimtuhumu kumjua kwa muda mrefu kama ndiye mke halali
wa mchungaji Imani na hata nyumbani kwao ameshawahi kuishi nao lakini
alikubali kumfungisha Imani ndoa na mwanamke mwingine.
MCHUNGAJI JUNGWA KIMYA
Mchungaji Jungwa hakuwa na la kuzungumza zaidi ya
kumung’unya maneno na kisha kusema alikuwa hawafungishi ndoa isipokuwa
alikuwa akiwabariki.
MAJIBU YAZIDI KUTIBUA
Majibu ya Mchungaji Jungwa yalimfanya mwanamke huyo azidi kuwa mbogo na kuwaanzishia kasheshe hapohapo madhabahuni.

Akihitimu masomo.
AHAMIA KWA MAMA MKWE
Elizabeth baada ya kuwavaa maharusi hao, aliangalia
mabenchi ya mbele na kumuona mama mdogo wa bwana harusi aitwaye Anna
Yona ambapo naye alimvaa na kumshutumu kuwa mama mkwe mnafiki anayejua
kuwa mwanaye ana mke, watoto na wajukuu naye lakini amekubali kutoroka
kutoka Mbeya kuja Dar kuhudhuria ndoa hiyo.
Katika varangati hilo, mama mkwe huyo aliyekaa na dada wa
bwana harusi waliishia kushika tama wakati wakisemwa na mkwe wao
Elizabeth.
MCHUNGAJI KIONGOZI AINGILIA
Katika kunusuru machafuko, mchungaji kiongozi wa kanisa
hilo aliingilia kati sakata hilo kwa kuwaomba watu watulie ili barua
hiyo ya mahakama isomwe vizuri kanisani hapo.
Kijana mmoja aliisoma barua hiyo iliyoonesha walikuwa na
mgogoro wa ndoa na kwamba walitakiwa kufika mahakamani Machi 5, mwaka
huu kujadili ndoa hiyo.
Alipofika kwenye kipengele hicho, waumini wote walisikika
wakimlaumu bwana harusi huyo kufunga ndoa hiyo kabla ya tarehe ya shauri
hilo.
Mke aliyekimbiwa.
NDOA YAKWAMA
Baada ya hapo mchungaji kiongozi aliamrisha ndoa hiyo ivunjwe na maharusi hao watarajiwa na watu wengine wote watawanyike.
Akizungumza na wanahabari wetu, Elizabeth alisema
kinachomuuma ni kwamba wametoka mbali sana na mumewe huyo ambapo
wamebahatika kupata watoto wanne na wajukuu wawili.
“Mbaya zaidi mume amechukua ng’ombe wangu nasikia ndiyo
amekwenda kumlipia mahari hiyo mwanamke. Yaani inaniuma sana,” alisema
mwanamke huyo.
Gazeti lilizungumza na mchungaji aliyekuwa akifungisha ndoa
hiyo ambapo alisema yeye alikuwa hawafungishi ndoa isipokuwa alikuwa
akiwabariki kwakuwa walishaanza kuishi.
Wanahabari wetu walipokuwa wakitaka kuwahoji maharusi,
mpambe wa bibi harusi aliwavamia na kuwanyang’anya kamera kitendo
kilichozua purukushani nyingine kanisani hapo huku msimamizi wa bwana
harusi naye akichimba mkwara.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kuwapora kamera waandishi na pia waandishi wetu hawakufanikiwa kuhojiana na bwana harusi huyo.