Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme ameagiza kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani wafanyakazi wote wa kitengo cha hifadhi y...
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme ameagiza
kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani wafanyakazi wote wa kitengo
cha hifadhi ya chakula cha taifa NFRA kanda ya Songea waliotajwa
kuhusika na utoroshwaji wa mahindi ya serikali zaidi ya gunia 1000 na
kuyahifadhi kwenye ghala la mfanyabiashara binafsi kinyume cha sheria.
Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma chini ya mkuu
wa mkoa Christina Mdeme walifanya ziara ya kushitukiza baada ya kupata
taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna mahindi yaliyowekwa kwenye
magunia ya serikali yanashushwa na kupekiwa upya kwenye mifuko ya
kawaida nyakati za usiku na kuyahifadhi kwenye ghala la mfanyabiashara
binafsi aliyefahamika kwa jina la Lotary Nkondola Safina.
Walinzi wa godauni hilo wamesema kuwa walipigiwa simu na
mmiliki wa ghala kuwa kuna mahindi yanaletwa ya NFRA hivyo wasiondoke
ambayo yametoka kituo cha Mgazini Peramiho na mengine makao makuu ya
NFRA Songea magari manne yalihusika kubeba mahindi hayo Semtrela mbili
na fuso mbili.
Meneja wa kitengo cha hifadhi ya chakula cha taifa NFRA
kanda ya Songea Amos Mtafya amesema mara kadhaa wanatumia godauni hilo
kuhifadhia mahindi ya serikali kutokana na uhaba wa maghala ya serikali.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa alitoa amri ya kutaifisha
mahindi yote yaliyokuwemo kwenye ghala hilo na kuwa mali ya serikali
pamoja na kukamatwa kwa wahusika meneja wa NFRA Amos Mtafya,mtunza
maghala Mariamu Mpangala na mhasibu Lugano Moses,wengine ni wafanyakazi
wa godauni Beda Kinyero,mmiliki wa godauni Lotary Nkondora,Yodan Nchimbi
na mlinzi Ado Ntuka.