Na Veronica Mheta, Arusha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha makazi ya askari poli...
Na Veronica Mheta, Arusha
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kuwa serikali
itaendelea kuboresha makazi ya askari polisi ili waweze kuishi kwenye
mazingira mazuri na kufanya kazi kwa weledi.
Mwigulu aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akitembelea nyumba mpya
zinazoendelea kujengwa za polisi baada ya zile za awali kuungua kwa moto.
Alisema serikali itaendelea kuboresha nyumba za askari wote nchini kwa
kujenga kwa awamu na hivi sasa serikali imeweka mkazo katika ujenzi wa
nyumba hizo za familia za watu 36 waweze kurudi kwenye makazi yao ya
uhakika.
Alitoa pole kwa familia zilizounguliwa na moto huo na kusisitiza kuwa ndani
ya mwezi huu nyumba hizo zinazotakiwa kukamilika ili familia hizo ziweze
kuishi kwenye nyumba hizo ambazo zimeungua hapo awali.
"Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
katika juhudi za kuhakikisha wanajenga kwa haraka nyumba hizi ili
kuhakikisha makazi ya askari yanaboreshwa natutaendelea kujenga nyumba za
askari wengine kadri tutakavyoweza"
Aliwapongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salam, Paulo Makonda kwa juhudi zao za kuhakikisha wanasogeza huduma
za maendeleo kwa wananchi wao kwa kushirikiana na wadau.
Pia alipoulizwa swali na waandishi wa habari ni kwanini sasa wasingeona
umuhimu wa kutumia kodi wanazokusanya kupitia askari wa Usalama barabarani
ili kutenga fedha kila mkoa kwaajili ya kujenga nyumba za askari hao
alisema wamechukua wazo hilo na watalifanyia kazi ili kuhakikisha askari
hao wanakuwa na nyumba za uhakika.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, CharlesMkumbo alishukuru Rais John
Magufuli kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa nyumba hizo sanjari na wadau
mbalimbali kwa michango yao ya hali na mali katika kuhakikisha maaskari hao
wanapata makazi mazuri.
Naye mmoja kati ya wadau hao ambaye ni mmoja kati ya wamiliki wa Kampuni ya
Madini ya Tanzanite One, Hussein Gonga alisema kama wadau wa maendeleo
wamemua kusaidia ujenzi wa nyumba za askari 18 kati ya 36 huku nyingine
zikijengwa na serikali na wanatarajia nyumba hizo kukamilika muda wowote
kuanzia sasa.
Pia alisema ujenzi wa nyumba hizo utagharimu zaidi ya sh,milioni 400 huku
wakipongeza ushirikiano uliopo kati ya Rc, Mrisho Gambo na wadau mbalimbali
wa maendeleo na kusisitiza kuwa wadau hao wanashirikiana kwa pamoja
kuhakikisha maendeleo Mkoa wa Arusha ya nakua kwa kiwango cha juu