Kenya inajiandaa kutimiza ndoto kubwa ya kisayansi leo Ijumaa. Chombo cha Satelaiti kilichoundwa nchini humo kitarushwa katika anga ...

Kenya inajiandaa kutimiza ndoto kubwa ya kisayansi leo Ijumaa. Chombo cha Satelaiti kilichoundwa nchini humo kitarushwa katika anga za juu hii leo kutoka nchini Japan.
Wanasayansi wa anga za juu kutoka Kenya waliokiunda chombo
hicho tayari wako katika makao ya Uchunguzi wa Sayansi ya Anga za juu
nchini Japan, (JAXA) ambapo chombo hicho kitarushwa kutoka huko.
Nchini Kenya kwenyewe raia wataweza kufuatilia shughuli
hiyo moja kwa moja kwenye mtandao wa You Tube, na sherehe maalumu ya
kushuhudia imeandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi.
Satelaiti hiyo ndogo ni ya thamani ya dola milioni moja -
gharama inayoonekana kuwa ndogo kifedha kwa kiwango cha sayansi ya anga
za juu.
Imebandikwa kamera mbili pamoja na vyombo vya kunasa na kupeperusha sauti.
Wahadhiri wa vyuo vikuu wanasema satelaiti hiyo inaweza
kutoa huduma tofuati ikiwemo kukusanya taarifa zitakazosaidia katika
kilimo na usalama, kutabiri hali ya hewa na hata kukabiliana na majanga.
Kenya kwa sasa inakabiliwa na janga la mafuriko ambalo limesababisha maafa makubwa.
Takriban watu mia mbili wamepoteza maisha yao, huku wengine zaidi ya laki mbili wamepoteza makaazi yao.
Huenda ufanisi katika uzinduzi wa satelaiti hii utaisaidia
serikali pakubwa katika kujitayarisha kupambana na majanga ya aina hiyo.
Uzinduzi wa satelaiti hiyo leo unatokana na ushirikiano
kati ya Idara ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, afisi ya
masuala ya anga za juu ya Umoja wa Mataifa, na Shirika la utafiti wa
anga za juu la Japan.
Kenya itaanza kushughulika kuunda satelaiti kubwa na bora zaidi iwapo uzinduzi wa leo utafanikiwa.



