Kifo cha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Konstebo Kulwa Gilbert, aliyepigwa risasi kwa bahati mbaya na mwenzake, kimezua ms...

Kifo cha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Konstebo Kulwa Gilbert, aliyepigwa risasi kwa bahati mbaya na mwenzake, kimezua mshtuko kwa ndugu, jamaa, askari wenzake na majirani aliokuwa akiishi nao nyumbani kwake, Ukonga-Mazizini jijini Dar,Gazeti la Uwazi pekee ndilo lenye mkasa mzima wa tukio hilo.
NI SINZA JIJINI DAR
Tukio hilo la kusikitisha lililotokea Jumanne ya wiki
iliyopita, majira ya jioni wakati afande Kulwa na FFU wenzake wakiwa na
askari wa kampuni binafsi ya ulinzi wakishusha pesa kwa ajili ya
kuziweka kwenye mashine ya ATM ya Benki ya CRDB iliyopo Sinza-Mori
pembezoni mwa Kituo cha Mafuta cha Big Bon, jijini Dar.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Uwazi kuwa, wakati
maafande hao wakiwa kwenye harakati za kushusha pesa hizo karibu na
mashine hiyo, kulikuwa na askari wa JWTZ aliyekuwa akitaka kutoa pesa
kwenye mashine hiyo hivyo afande Kulwa na wenzake walimuamrisha aondoke
haraka eneo hilo kwa sababu za kiusalama.
MASHUHUDA WASIMULIA
Kwa mujibu wa mmoja wa mashuhuda hao, Jimmy Kaishozi, mkazi
wa Sinza-Meeda, mwanajeshi huyo, baada ya kupewa amri ya kuondoka
haraka eneo hilo, aliona kama amedharauliwa na askari hao hivyo
aliwataka wamwambie kistaarabu na siyo kumwamrisha.
Kaishozi alisimulia kuwa, hali hiyo ilizua malumbano kati
ya askari hao na mwanajeshi huyo ambapo Kulwa alimfuata jamaa huyo akiwa
na bunduki mkononi huku akimuelekezea ambapo mwanajeshi huyo aliikamata
na kuelekezea mtutu juu, jambo lililoonekana kuwa alikuwa na utaalam wa
masuala ya silaha.

Kamanda Mambosasa.
“Kitendo hicho kilizidisha taharuki ambapo askari mwingine
wa FFU naye alitoka kwenye gari lililokuwa limebeba pesa na bunduki
nyingine na kumlenga mwanajeshi huyo, lakini katika hali iliyoonekana
kama bahati mbaya, risasi hizo zilimpata afande Kulwa na nyingine
ilimlenga mwanajeshi huyo.
“Hapo mapambano yalizidi kukolea kama sinema ya kivita
ambapo askari aliyekuwa akilenga shabaha, alipoona amempiga mwenzake,
aliikoki tena bunduki na kumpiga risasi nyingine mwanajeshi huyo ambapo
afande Kulwa na mwanajeshi huyo, wote walianguka chini na kuanza
kutapatapa huku wakitokwa na damu nyingi.
“Ilichukua muda wakigaragara chini hadi walipofika askari
wa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama (Mabatini) na kuwachukua, sijui
walipelekwa wapi,” alisimulia Kaishozi.



