KIONGOZI Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo,Zitto Kabwe,ameeleza kusikitishwa kwake na matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea kutokea...
KIONGOZI Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo,Zitto
Kabwe,ameeleza kusikitishwa kwake na matukio ya utekaji na mauaji
yanayoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuitaka
Serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha matukio
hayo na taarifa ziwekwe wazi ili jamii ijue.
Amesema kuwa matukio hayo kwa sasa yamekuwa yakishika kasi
na yameonekana kuwa ni matukio ya kawaida tu ili hali damu za Watanzania
wasio na hatia imekuwa ikimwagika kila kukicha katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma mjini kupitia
ACT-Wazalendo aliyasema hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari,alipokuwa katika ziara yake na kutembelea Kata
zinazoongozwa na Madiwani kupitia chama hicho.
Akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa,pamoja
na viongozi wengine ngazi ya Taifa na mikoa atakayotembembelea alisema
kuwa lengo la ziara yake hiyo ni kuwashukuru wananchi wa Kata hizo kwa
kuwapa dhamana ya kuongoza kata hizo katika uchaguzi mkuu wa oktoba
2015.
“Pia tutashiriki kazi za maendeleo,kushawishi utekelezaji
wa maono ya azimio la Tabora kwenye miradi ya maendeleo,kutafuta
majawabu ya changamoto zinazowakabili,kusikiliza kero zao na kuzifikisha
katika mamlaka husika,kukagua utendaji wa madiwani,ikiwa ni pamoja na
kusisitiza uwazi,uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi kwenye
masuala yote yahusuyo Kata zao”alisema Zitto.
Kadhalika alizungumzia hatua ya wao kukamatwa na polisi
walipokuwa katika ziara yao ya mkoani Morogoro wakitokea Mkoa wa Pwani
kuwa walishishwa kuendelea na zira yao katika Mkoa huo baada ya
kukamatwa na polisi na kulazimika kulala ndani kabla ya kuachiwa kwa
dhamana jana ambapo leo wataendelea na zira yao katika kata ya Sale
Wilayani Ngorongoro Mkoani hapa ambapo wana madiwani wawili.
Akizungumzia hatua yao ya kukamatwa na polisi alisema kuwa
ni baada ya wao kuamua kutembea kwa miguu kwa mwendo mrefu kuelekea
Kata ya Luela kutokana na kukosekana kwa barabara ya kuingia na kutoka
katika kata hiyo na ndipo walipokamatwa na polisi kwa maelezo kuwa
wametumwa na wakubwa wao wa kazi kwa madai kuwa nimefanya mkutano bila
kibali ilihali hakuna mkutano wowote tulioufanya.



