Serikali imetangaza utaratibu mpya wa kuingia katika machimbo ya Tanzanite yaliyopo Mererani ambapo kuanzia Februari 15 ni lazima mtu a...

Serikali
imetangaza utaratibu mpya wa kuingia katika machimbo ya Tanzanite
yaliyopo Mererani ambapo kuanzia Februari 15 ni lazima mtu awe na
kitambulisho maalumu.
Akizungumza
na wachimbaji wa madini hayo jana Februari 13 mjini hapa, Kamishna na
Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alisema vitambulisho
vitakavyotakiwa ni vile vinavyotolewa na Wizara ya Madini.
Juma alisema hadi sasa ni vitambulisho 6,000 ambavyo tayari vimetolewa na katika machimbo hayo kuna wachimbaji zaidi ya 15,000.
"Baada ya ujenzi wa ukuta kukamilika sisi kama wizara tutaanza Februari 15 kudhibiti kuingia migodini," alisema.
Alisema
wamiliki wa migodi yote, wachimbaji na madalali wa madini pamoja na
watu wengine ambao watataka kuingia kwenye eneo lililozungushwa ukuta
lazima wawe na vitambulisho.
Mkuu
wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema agizo hilo la Serikali
halina utani, hivyo ni lazima wanaotaka kuingia migodini wafuate
sheria.
Alisema
lengo ya mpango huo ni kuhakikisha madini hayatoroshwi na pia Serikali
inapata stahiki zake kabla ya madini kutoka nje ya uzio.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Sadiki Mnenei
alisema wanaunga mkono mpango wa vitambulisho, lakini wanaomba muda
zaidi wa kuzuia wasio na vitambulisho hadi Machi mosi.
"Ili
kutoathiri kazi zetu tunaomba utaratibu mpya kuanza mwezi ujao kwani
gharama za kitambulisho ni kubwa kwa kuwa kila mchimbaji anatakiwa kutoa
Sh3,500 na mmiliki wa mgodi Sh5,000," alisema.
Alisema kwa wastani mgodi mmoja una zaidi ya wafanyakazi 100, hivyo wote kuwapa vitambulisho wakati mmoja ni vigumu.



