Kifo cha Mwanafunzi wa Chuo kikuu nchini Kenya kimezuaa shutuma mpya za mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi nchini humo...

Kifo cha Mwanafunzi wa Chuo kikuu nchini Kenya kimezuaa
shutuma mpya za mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi
nchini humo.
Ripoti zinasema Evans Njoroge, mwanafunzi ambaye alikua
kiongozi Chuo kikuu cha Meru nchini humo, aliuawa kwa kupigwa risasi na
anayedaiwa kuwa polisi.
Mwandishi wa BBC, Ferdinand Omondi anasema pichaza mwili wa
kijana huyo, damu yake ikionekana imetapakaa kote, zimekuwa zikisambaa
kwenye mitandao ya kijamii huku raia wa Kenya wakighadhabishwa na kile
walichodai kuwa mauaji yanayotekelezwa na polisi.
Evans alipigwa risasi Jumanne wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakilalamikia ongezeko la ada dhidi ya chuo cha Meru.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimemnukuu shuhuda mmoja
akisema polisi walimkimbiza Evans wakamfikia kisha mmoja wao akampiga
risasi na kuondoka.
Mkuu wa polisi Jenerali Joseph Boinnet ameamuru kufanyika
uchunguzi kuhusu kifo hicho baada ya kuwepo kwa wanasiasa na makundi ya
wanaharakati waliokuwa wakitaka mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na polisi
kukoma mara moja.
Shirika huru la kiraia linalofuatilia shughuli za polisi (IPOA) limesema limewatuma maafisa wake kuchunguza tukio hilo.
Mwanafunzi huyo aliuawa katika eneo la Nchiru, eneo la
Tigania West katika jimbo la Meru ambalo linapatikana katika eneo la
Mlima Kenya.
IPOA wamesema maafisa wa uchunguzi wametukwa kwa lengo la:
"kuchunguza kuhusu yaliyotokea wakati wa mauaji hayo na iwapo kuna mtu
anayefaa kulaumiwa, na kuhakikisha afisa yeyote wa polisi
atakayepatikana na hatia anawajibishwa kisheria."
Wakenya mtandaoni wamekuwa wakishutumu mauaji hayo.
Shutuma hizi mpya zimekuja siku kadhaa baada ya shirika
linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch kuwasilisha ushahidi
mpya kuwa polisi nchini Kenya waliua watu takriban 23 wakati wa kipindi
cha marudio ya uchaguzi nchini humo mwaka jana.
Kwa mujibu wa ripoti,uchunguzi umebaini kuwa wengi wa waathirika walifyatuliwa risasi na silaha za nguvu.
Polisi wameendelea kukana shutuma hizo.



