Serikali ya Rwanda kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano nchini humo (RURA), imekifungia kituo cha redio ya kidini cha ...

Serikali ya Rwanda kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Mawasiliano nchini humo (RURA), imekifungia kituo cha redio ya kidini
cha Amazing Grace 105.1 FM kurusha matangazo kwa kipindi cha mwezi
mmoja pamoja na kulipa faini ya faranga milioni 2 sawa na Tsh milioni 6,
baada ya redio hiyo kurusha matangazo yaliyowadhihaki wanawake kwa
kuwataja kuwa ndiyo chanzo cha matatizo duniani.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa mnamo Tarehe 29 Januari 2018
Mchungaji wa Kanisa la Kisabato, Niyibikora Nicholas akitangaza injili
kupitia kituo hicho cha redio alisikika hewani akisema wanawake ni moto
wa kuotea mbali kwani ndo chanzo cha maovu na migogoro isiyoisha
duniani.
Mchungaji huyo akiwa LIVE hewani aliendelea kusema kuwa
hata Mungu hawapendi wanawake, kwani mwanamke hajawahi kuwa mtu mwema
tangu enzi za bustani ya edeni ambapo alikula tunda alilokuwa ameambiwa
asile na kumshawishi na mumewe kufanya dhambi.
Mamlaka hiyo ilichambua mahubiri yake yote ambapo imeeleza
kuwa maudhui yote yalitoa mifano lukuki ya kwenye biblia inayowaelezea
wanawake kuwa ni watu wabaya huku mchungaji huyo akiwataka wanaume
wasiwaamini wanawake kwani wanawake ni watu wabaya.
Mhubiri huyo alizua mjadala mzito kwenye mitandao ya
kijamii nchini Rwanda na kuwakasirisha wanawake ambapo Mwavuli wa
Utetezi wa Haki za Wanawake Rwanda (Profemmes Twese Hamwe) na Jukwaa la
Waandishi wa Habari wa Kike Rwanda (ARFEM) walipaza sauti zao kutaka
achukuliwe hatua kwa tuhuma za uchochezi wenye misingi ya kijinsia na
kulenga kusababisha mtafaruku kwenye jamii.
Tayari Ofisi ya Mwendeshaji Mkuu wa Mashtaka imeliagiza
jeshi la polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai kuanza
upelelezi juu ya madai yanayomkabili Mchungaji huyo.
Chanzo:The New Times



