Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalim...

Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha
muswaada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya
Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (The Public Service Act) itakayowezesha
muda wa kustaafu kwa Wahadhiri waandamizi, Maprofesa na Madaktari
Bingwa kuwa miaka 60 kwa hiari na lazima miaka 65.
Akizungumza wakati akiwasilisha muswaada huo Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amesema kuwa marekebisho katika
jedwali yanapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 25A ambacho
kinaainisha kuhusu umri wa kustaafu ambapo kwa sasa sheria ilivyo haina
masharti hayo isipokuwa umri wa kustaafu umetajwa katika sheria
zinazoanzisha mifuko ya hifadhi za jamii.
Aliongeza kuwa, uzoefu umeonyesha kuwamba Maprofesa na
Wahadhiri waandamizi wa vyuo Vikuu vya Umma pamoja na madaktari Bingwa
wa Binadamu wa Hospitali za Umma wamekuwa wakihitajika kuendelea kutoa
huduma, utaalamu na uzoefu wao licha yakufikisha umri wa miaka 60 kwa
sasa ya kustaafu na hivyo kulazimika kuajiriwa na Serikali kwa mikataba.
Hatua yakuwaajiri wataalamu hao kwa mikataba baada ya
kustaafu imetajwa kuongeza gharama kubwa kwa Serikali ambapo muswaada
ulipitishwa unawezesha Serikali kuokoa Kiwango kikubwa cha fedha
zilizokuwa zikitumika katika kuwalipa wataalamu wao mara baada ya
kustaafu ili waweze kufanya kazi kwa mikataba.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknplojia mhe.
Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa anaunga mkono hoja yakuongeza
umri wa kustaafu kutoka miaka 60 kwa lazima hadi 65 na kutoka miaka 55
kwa hiari hadi miaka 60.
Aliongeza kuwa Serikali inayo mikakati ya makusudi
yakuwaendeleza wataalamu wa kada zenye uhaba wataalamu wabobezi ili
kuziba pengo lililopo.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano
wake wa 10 kikao cha 1 limepitisha muswaada wa marekebisho ya sheria
mbalimbali nne ambazo ni Sheria ya Ufilisi, sura ya 25, Sheria ya
Bajeti, sura ya 439, Sheria ya Ardhi, sura ya 113 na Sheria ya Utumishi
wa Umma, sura ya 238.



