Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla jana Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya watuhumiwa wa ujangili ambao w...

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla jana Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni wamiliki na washirika wa Kampuni za uwindaji wa kitalii na kuwapa siku saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe katika ofisi za Wizara hiyo Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa maelezo kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk.
Kigwangalla ametaja baadhi ya tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria
na taratibu za uwindaji wa kitalii kuwa ni uwindaji haramu,
uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji pasipo kufuata sheria,
udanganyifu kwenye kujaza fomu za uangalizi, rushwa, uhalifu dhidi ya
rasilimali za wanyamapori na uhujumu uchumi.
Alitaja tuhuma zingine kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za
uwindaji (kupiga wanyama usiku, kuwinda wanyama bila kujali umri, kupiga
wanyama nje ya maeneo waliyopewa), kukutolipa tozo mbalimbali za
maendeleo za jamii kwenye vijiji jirani na maeneo wanaoendesha biashara
ya uwindaji, kushindwa kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.
Dk. Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu
Pasanis na wenzake ambao wanamilikia kampuni ya Berlette Safari
Corporation Ltd na Ngugu Shein Ralgi na wakurugenzi wenzake wa kampuni
ya Game Frontiers of Tanzania Ltd.
Wengine ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya
Mkwawa Hunting Sfaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa
Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania Ltd
na Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, na Ndugu Awadh na wenzake ambao
wanamiliki kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles Safaris Ltd.
Aliwataja washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu
Robert, Ndugu Solomon Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul
Ligagabile na mtumishi wa Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex
Aguma.
Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa Ilani ya siku
30 kwa watu mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu Wastaafu waliovamia
kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha wafike kwa
Kamishna Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao
halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki
wake halali.
“Natoa ilani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambaye anajua
alivamia kiwanja katika eneo hili ambalo lina hati namba 4091 kilichopo
Njiro, Arusha, haraka sana ajipange kupeleka taarifa zake mbele ya
Kamishna wa Ardhi kabla hatujachukua hatua nyingine za kisheria, hati
iliyoko pale ipo katika jina la Bodi ya Utalii Tanzania japo wao wanadai
wana hati nyingine.
“Wengi wao wamejenga nyumba za kudumu katika eneo lile, na
wengine ni viongozi waliokuwa mawaziri wakuu wastaafu nao wana viwanja
katika eneo hilo na wamejenga nyumba zao katika eneo hilo,” alisema Dk.
Kigwangalla.
Alisema kiwanja hicho kilichokuwa na ekari zaidi ya 40
kilikuwa kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya
Bodi ya Utalii Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari
Lodges na baadae kikauzwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa Jeshi
la Polisi nchini kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wanne wanaojihusisha
na mtandao wa ujangili pamoja na kupanga njama zilizopelekea mauaji ya
Mhifadhi wa Wanyamapori Ndugu Wayne Lotter, raia wa Afrika ya Kusini
ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni Pams Foundation, aliyeuawawa eneo
la Chole Masaki Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana.
“Natoa siku saba kwa wenzetu wa jeshi la Polisi wachukue
hatua dhidi ya watu wanne, ambao mimi majina yao ninayafahamu ambao
miongoni mwao watatu wanahusika na kuendesha biashara ya ujangili, na ni
watu wakubwa, ni matajiri wakubwa na wana mitandao mikubwa ya ujangili.
“Ninafahamu taarifa hizi polisi wanazo lakini hawajachukua
hatua za kuwakamata watu hawa na kuwafikisha kwenye macho ya sheria,
muda ni mrefu na sisi wenye taarifa hizi sasa tumeanza kuchoka
kusubiri.
“Hawa watu wanne walihusika kupanga njama ambazo
zilipelekea kusababisha mauaji ya kikatili ya Mkurugenzi wa Kampuni ya
Palm Foundation, Ndugu Wayle Lotter mwezi Agosti mwaka jana eneo la
Chole Masaki mwezi Agosti mwaka jana.
“Nataka ndani ya siku hizi saba wawe wamechukua hatua na
kama hawatochukua hatua manaake tutajua wana vested interest (maslahi)
kwahivo tutaenda kuripoti kwa Amiri Jeshi mkuu ambaye ni Mhe. Rais
aliyetutuma kazi ya kusimamia sekta hii,”. Alisema Dk. Kigwangalla.



