Kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kis...

Kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, imeahirishwa hadi Februari 26.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas jana alimueleza Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi imepangwa kwa ajili ya kutajwa na
kwamba hadi sasa hawajajua hali ya mshtakiwa wa nne, Lissu.
Kesi hiyo ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa
ushahidi wa upande wa mashtaka, inamkabili Lissu na wenzake Simon Mkina,
Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano
likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti
ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es
Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha
taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja
Zanzibar.’
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika
jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio
lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.



