Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. John Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli leo wameshiriki Misa ya Krismasi katika Kanisa K...
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. John Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli leo wameshiriki Misa ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani Singida.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Baba Askofu wa Jimbo la Singida Askofu Edward Mapunda mara baada ya Ibada ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani Singida.
Rais amewahi kusali katika kanisa hilo kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana huku akimkumbuka Sister mmoja aliyemkabidhi rozali na kumuahidi kushinda nafasi ya urais katika uchaguzi huo.
Akizungumza katika ibada hiyo Rais Magufuli amesema rozali hiyo alikuwa anazunguka nayo kwenye ziara zake za kampeni hadi mwisho na kufanikiwa kupata kura za kutosha zilizompa ushindi.
Amesema kusali hapo ni moja ya sababu kubwa ya siri ya ushindi wake, na hivyo kuungana na wakazi wa mkoa wa Singida na watanzania wote kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Magufuli ametumia fursa hiyo kuwataka watanzania kutumia Sikukuu ya Krisimasi kuimarisha upendo, kuvumiliana na kutobaguana, kwani njia ya upendo itasaidia taifa kujipatia maendeleo.
Aidha, amewataka wakulima kuhakikisha wanazitumia vizuri mvua za sasa katika kuchapa kazi ya kilimo kwa nguvu zote pamoja na kulima mazao yanayostahimili ukame.
Amesema Sikukuu ya Krismasi kunadhihirisha kauli mbiu ya 'hapa kazi tu', kwani Yesu Kristo alikuwa fundi mzuri wa useremala hivyo kuwataka watanzania kumuiga, na pia akiwataka wakazi wa mkoa wa Singida, kuongeza uzalishaji wa zao la alzeti ili kuviwezesha viwanda vya kukamua mafuta ya alzeti kupata mbegu nyingi.
Awali Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Edward Mapunda, amewakumbusha wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wanatunza mazingira ili yaweze kuwatunza na kuwaepusha na ukame wa mvua.
Baba Askofu wa Jimbo la Singida Askofu Edward Mapunda akimuombea na kumbariki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Ibada ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani Singida.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia waumini wa Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu mkoani Singida mara baada ya kushiriki Misa ya Krismasi katika kanisa hilo mkoani Singida



