MGONGANO wa kiutawala umeanza kufukuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, anaandika Happiness Lidwino. Cha...

MGONGANO wa kiutawala umeanza kufukuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, anaandika Happiness Lidwino.
Charles Kuyeko, meya wa manispaa hiyo ameeleza kwamba, hayuko tayari kuona viongozi wanaotokana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakiuka mipaka ya taratibu za kazi kwa sababu za kiitikati ama dharau.
Meya huyo anayetokana na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesema, hatua ya Isaya
Mgurumi, mkurugenzi wa halmashauri hiyo alilotoa juzu kuwatimua
wafanyabiashara wamachinga mjini bila kufuata taratubu inaonesha dharau.
Amesema, Mgurumi amefanya hivyo bila
kumuhusisha meya na madiwani wa manispaa hiyo. Kutokana na
kutishirikishwa kwao, leo wametengua uamuzi wa mkurugenzi huyo.
Katika kikao cha dharura kilichoitishwa leo na meya huyo, madiwani wa CCM hawakuhudhuria ambapo waliohudhuria ni madiwani kutoka kwa vyama upinzani.
Madiwani hao wamewataka wamachinga kutoondoka katika maeneo yao hadi watakapotafutiwa maeneo manzuri ya kufanyia biashara, huku wakimtaka mkurugenzi kurudi mezani kwa ajili ya mazungumzo.
Mgurumi juzi wakati akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam, aliwataka wamachinga waliopo maeneo
ya mjini hususan barabarani kuondoka mara moja ndani ya siku tatu.
Pia aliwapangia maeneo ya kwenda kufanyabiashara zao ambayo ni Ukonga Magereza, Muslimu Tabata, Kigogo Fresh na Kivule huku akiwatisha kwamba, atakayekaidi tamko hilo, mgambo na askari wa mabomu watafanya kazi yake.
Akizungumza na waandishi leo ofisini
kwake Kuyeko amesema, amesikitishwa na tamko hilo ambalo hakushirikishwa
kama kiongozi wa manispaa hiyo.
Amesema, badala ya kushirikishwa, aliletewa tamko hilo ili kutolea msisitizo.
“Nashindwa kuwaelewa viongozi wenzetu kwa kushindwa kutushirikisha masuala ya maendeleo katika manispaa tunayoiongoza wote.
“Yaani baada ya kufanya uamuzi na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa basi sisi wengine ambao tupo kwa niaba ya wananchi tunaonekana hatuna maana tena.
“Baada ya kutoa tamko ndio naambiwa nitoe msisitizo, hiyo ni dharau na ndio maana sikufanya hivyo,” amesema Kuyeko.
Amesema, licha ya yeye kutopewa taarifa
hata madiwani wa maeneo ambayo mkurugenzi amewataka wamachinga kwenda
hawana taarifa juu ya ugeni huo na kwamba, maeneo ya masoko hayatoshi
kubeba watu wengi.
Patrick Assenga, Diwani wa Kata ya Tabata anasema, ameshangazwa na hatua mkurugenzi kufanya uamuzi kabla ya kuzungumza na viongozi wa maeneo husika.
“Hapa katika kata yangu soko halina vyoo
wala maji ya kutosha, hata hivyo eneo ni finyu kutokana na kuwepo kwa
shughuli nyingi za CCM ikiwepo ofisi yake na maegesho ya magari yao
ambapo tumepiga kelele kwa muda mrefu waondoe shughuli zao lakini hadi
sasa wamekaidi halafu wanaleta habari hizi,” amesema.
Stevene, Msigwa Mwenyekiti wa Wamachinga Wilaya ya Ilala amesema kuwa, wafanyabiashara hawana imani tena na serikali kwa kuwa, licha ya kushirikiana katika mambo mengi lakini imeamua kuwachukulia hatua kwa vitisho pasipo kuwashirikisha kwenye uamuzi huo.
“Ni vema wangetuita tufanye mazungumzo
kabla ya kutuchukulia hatua kwani sisi ni binadamu na tuna majukumu,
kuhamisha biashara kunahitaji maandalizi.
“Hatukaidi kuondoka ila hatutaondoka hata watumie mabomu hadi pale watakapotupatia maeneo manzuri yenye miundombinu mizuri kwani tunalipa kodi zetu,” amesema Msigwa.
Hata hivyo, madiwani waliohudhulia kikao hicho cha dharura wamesema, hawaina imani tena na mkurugenzi kutokana na maamuzi yake yasiyo shirikishi ambayo yanaonekana kuwa na shinikizo kutoka kwa Makonda.
Pia wamesema, endapo kesho shughuli hiyo itaendelea, watachukua hatua kali kutokana na kutosikilizwa.



