Rais Dkt John Magufuli akigonganisha glasi na Rais Paul Kagame wa Rwanda RAIS Paul Kagame wa Rwanda amempongeza na kumsifia Rais Jo...
![]() |
| Rais Dkt John Magufuli akigonganisha glasi na Rais Paul Kagame wa Rwanda |
RAIS Paul Kagame wa Rwanda amempongeza na
kumsifia Rais John Magufuli kutokana na mfumo wa uongozi wake hasa nia
yake thabiti ya kupambana na ufisadi.
Kagame aliyasema hayo juzi katika hafla ya
chakula cha jioni aliyoiandaa kwa ajili ya mgeni wake, Rais Magufuli
aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika taifa hilo .
“Kwanza nataka ujue kuwa hapa ni nyumbani
kwa kaka yako. Tangu uchaguliwe kuwa Rais, uwepo wako umekuwa wa
kipekee, matendo na maneno yako yanaakisi maono yetu,” alisema Rais
Kagame.
Aidha, alisema jitihada na msimamo wa Dk Magufuli katika kupambana na tatizo la rushwa na ufisadi ni wa kupongezwa na kuigwa.
Akiwasili nchini humo juzi, Dk Magufuli
alisafiri umbali wa takribani kilometa 1,460 kwa barabara, ikiwa ni
ziara yake ya kwanza ya kikazi nje ya Tanzania tangu achaguliwe kushika
wadhifa huo Oktoba mwaka jana.
Msafara wa Rais huyo ulipokewa kwa shangwe
na wananchi wa Rwanda wakati ukipita kwenye mji wa Rusumo kwenda mpakani
mwa nchi ya Rwanda na Tanzania.
Baada ya kuwasili Rusumo ambako ni mpaka wa
Tanzania na Rwanda katika wilaya ya Ngara kwa Tanzania, Dk Magufuli na
mwenyeji wake walifungua majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa
Huduma za Mpak ani kilichopo upande wa Tanzania, kisha wakafungua daraja
la mto Kagera.
Dk Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth
Magufuli jana waliungana na wananchi wa Rwanda kuadhimisha kumbukumbu ya
miaka 22 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo vya
watu takribani milioni moja.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika eneo la
Gisozi mjini Kigali yalipo makumbusho ya mauaji ya Kimbari ambako Rais
Magufuli na mkewe wakiwa na mwenyeji wao Rais Paul Kagame na mkewe Mama
Janeth Kagame waliweka shada la mau katika eneo walipouawa idadi kubwa
ya wananchi wa Rwanda na pia wakawasha mwenge wa matumaini kwa
walionusurika katika mauaji hayo na kwa Taifa zima la Rwanda.
Pamoja na kupata historia ya mauaji hayo ya
kimbari, Rais Magufuli akiongozwa na mwenyeji wake alitembelea jumba
maalumu lililohifadhi kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha, ambako
alipata maelezo kutoka kwa wahifadhi wa makumbusho hiyo, na pia kujionea
picha na mabaki ya mifupa na mafuvu ya binadamu waliouawa.
Akizungumza baada ya kutembelea jumba hilo
la makumbusho, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na mauaji hayo
na kusema tukio hilo halipaswi kurudia.
“Haitatokea tena, hatuwezi kubadilisha
yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo ya sasa na yajayo, mauaji
haya hayapaswi kutokea tena,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ambaye aliingia nchini Rwanda
juzi ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani
Novemba 5, mwaka jana, aliondoka Kigali jana jioni na kurejea jijini Dar
es Salaam.




