Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. ZAIDI ya wakazi 547 wa Dar es Salaam wametekeleza agizo la kuhakiki silaha zao kam...
ZAIDI ya wakazi 547 wa Dar es Salaam wametekeleza agizo la kuhakiki silaha zao kama ilivyotolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda. Makonda alitoa agizo kwa kuwapa siku 90 wakazi hao kuhakikisha kwamba wanahakiki silaha zao.
|
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema kuwa tangu kutangazwa kwa agizo hilo wananchi wamejitokeza kwa wingi kuhakiki silaha.
Alisema jeshi hilo linaendelea kuwahimiza kutii agizo hilo kabla siku hazijaisha. “Wananchi wamejitokeza kwa wingi na jeshi likihitaji kutoa namba kwa kila silaha basi watapewa taarifa.
Tunajua kwamba wengi wanamiliki silaha za babu au baba zao hivyo wanatakiwa kuhakiki ili kujua mmiliki halali wa silaha hizo,” alisema Sirro. Pia aliwataka endapo kutakuwepo wananchi ambao hawatahakiki mpaka muda huo utakapoisha, watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Rais John Magufuli alikuwa wa kwanza kutii agizo la Mkuu wa Mkoa huo kwa kuhakiki silaha zake. Wakati huo huo, jeshi hilo limesema litashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha kwamba kunakuwa na ulinzi katika maeneo yao.
Kamanda Sirro alisema Mkoa wa Kipolisi wa Temeke umeonesha mfano kwa kuwa na vikundi vidogo vya ulinzi shirikishi ambavyo vimesaidia kupambana na panya road na vibaka. Alisema ni tofauti na mikoa mingine ya Kipolisi ya Ilala na Kinondoni ambao hawana vikundi vilivyosajiliwa na serikali za mitaa.
Alisisitiza kuwa ni vyema vikundi vya ulinzi shirikishi vinatambulika katika sheria ndogo ndogo za serikali za mitaa hivyo vilivyopo vikasajiliwe ili kutambulika kisheria. “Vikundi ambavyo havitasajiliwa havitatambulika kisheria. Hivyo ninaomba mikoa mingine ya kipolisi iige juhudi hizi kuhakikisha kwamba hali ya usalama inakuwa shwari,” aliongeza Kamanda Sirro.



