Kamati ya Wataalamu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kutokea maporomoko ya udongo,mawe na tope katika mlima Hanang' imebaini kuwa chanzo...
Kamati ya Wataalamu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha
kutokea maporomoko ya udongo,mawe na tope katika mlima Hanang' imebaini kuwa
chanzo kilikuwa mipasuko ya miamba iliyohifadhi maji ya mvua iliyonyesha
mfululizo kushindwa kuhimili na kusababisha udongo kuanza kuserereka na kuleta
maafa kwa wananchi .
Hayo yamebainishwa Jana Oktoba 7,2024 na Mkurugenzi wa
huduma za Jiolojia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt Ronald
Massawe wakati akitoa ufafanuzi wa matokeo ya utafiti wa kamati ya wataalamu
iliyoundwa na kitengo cha maafa ofisi ya Waziri Mkuu na kuwasilishwa kwa
wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.
Amesema mlima Hanang' ni miongoni mwa milima iliyopo
katika mkatiko au ufa wa Balanginda wa ukanda wa kaskazini wa bonde wenye
miamba yenye mipasuko mingi inayohifadhi maji ambayo siku chache kabla ya
kutokea maporomoko ya Disemba 3, 2023 ilijaa maji kutokana na mvua zilizonyesha
mfululizo iliyosababisha kumeguka na kuanza kuserereka na kusababisha maafa.
Uwasilishaji wa ripoti hiyo ya utafiti wa chanzo cha
maporomoko ya udongo na mawe kutoka mlima Hanang' imeenda sambamba na uzinduzi
wa nyaraka ya usimamizi wa maafa, ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Maafa Dkt Jim Yonaz aliyekuwa Mgeni rasmi ameelekeza wataalamu
wa Halmashauri ya Hanang kuzingatia ili kusaidia kupunguza athari ya maafa kwa
siku sijazo.
Inaelezwa kuwa ripoti ya kina ambayo tayari
imezinduliwa ilifanyika April 2024 na kukamilika Mei 2024.