Utangulizi : Kila mwanaume aingiapo katika mahusiano huanza uchunguzi kimyakimya, wakati wanawake wao huweza kuchunguz...
Utangulizi:
- Kila mwanaume aingiapo katika mahusiano huanza uchunguzi kimyakimya, wakati wanawake wao huweza kuchunguza kwa kuuliza au kudadisi.
- Mara mwanaume anapogundua kuwa mazingira aliyopo hatoyaweza basi huanza kufungasha virago vyake kimya kimya na akishafanya maamuzi ya kukukimbia basi utaona visingizo na sababu tele zisizo na mashiko zikimiminika. Kwa mfano utasikia maneno kama vile; “Mimi nahisi tofauti ya dini zetu itatusumbua huko mbeleni”, “Naona wazazi wangu wanakuwa wagumu sana kwenye mahusiano yetu”, “Ndugu zangu wamenishauri nisubiri kwanza”, “Nimepata nafasi ya kwenda kusoma mbali”, “Kwa sasa nashindwa kufanya maamuzi magumu maana nina mipango fulani ya maisha naifanyia kazi”, “Nahisi bado sijajipanga kifedha kuweza kuanza familia”.
- Kama hatotoa visingizio hivi basi anaweza kutafuta kitu anachojua fika kwamba hautokikubali na akaamua kukisimamia hicho ili ukikikataa uwe mwisho wa mahusiano yenu, kwa mfano atasema; “Mimi ninaona tuzae kwanza halafu baadae tutafunga ndoa” (hapa kama amejua fika kuwa wewe hauna mpango wa kuzaa nje ya ndoa), au atasema “Tuishi pamoja kwa sasa halafu nikiwa sawa tutaanza mchakato ya harusi”.
Fahamu kwamba: Sababu hizi zinaweza kujidhihiridha kwenye mahusiano
kabla ya kuingia kwenye ndoa au hata mkiwa kwenye ndoa na hivyo kusababisha
ndoa nyingi kuvunjika mapema sana, hususani zile zinazopasuka chini ya miaka
mitano.
Sababu:
- Wanapohisi au kuona utegemezi
Utegemezi huu unaweza kuwa katika maeneo mengi ya
maisha lakini wenye madhara sana ni utegemezi wa kiuchumi. Ingawa mwanaume
anajua kuwa anawajibika kwa mpenzi wake lakini mara nyingi huwa mwoga na mwenye
kuhamaki sana pale anapoona kila dakika anaombwa fedha au kuombwa msaada wowote
ambao kwa namna mmoja au nyingine utamgharimu fedha. Wanaume wengi hupendelea
na wanahisi usalama zaidi pale ambapo wapenzi wao wa kike wanaonyesha
kujitegemea au kujiweza katika baadhi ya mambo. Mara nyingine hata kama
mwanaume anaonyesha kuwa tayari kuwajibila kwa asilimia zote kwa mpenzi wake,
lakini bado ndani yake anatamani kuona ule utayari wa mpenzi wake kujisimamia
na kujitegemea. Wale wakinadada wenye tabia ya kuanza kuwakilisha shida zao
nyingi mbele ya wapenzi wao wa kiume kama vile wamewapenda ili wawe watatuzi wa
matatizo yao binafsi nay a familia zao pia, wakina dada hawa mara kwa mara
kupata shida ya kupendwa au hata kuchumbiwa mara nyingi na kuachwa pasipo kujua
kwanini wanaume wanawakimbia.
- Pale wanapohisi au kuona kuwa unawakwepa au kutowafurahia wazazi/ ndugu zake
Hata kama kuna changamoto fulani kutoka kwa ndugu
zake, wanaume wengi wanatamani kuona jitihada zako kwenye kuwa karibu na wazazi
au ndugu zake, na kama kuna vikwazo basi muwasiliane kwa pamoja katika namna ya
kuvishughulikia. Iwapo utaamua tu mwenyewe kuwakwepa au kujiepusha nao pasipo
sababu yenye mashiko, au ukaamua kumwambia wazi kuwa hauwapendi au hauwahitaji
ndugu zake basi utaona wazi hofu yake ya kuwa na wewe. Wako wakina dada
walioifahamu siri hii na utawakuta wakijipendekeza na kujipeleka zaidi kwa
wakwe au ndugu wengine wa mwanaume ili tu mpenzi wake wa kiume afurahi, ni
kweli wamefaulu katika hili lakini ni vema upendo wako ukawa halisi na sio ulio
wa uongo au feki.
- Wanapohisi au kuona dalili za mtu mbishi na mpinzani
Kwa kawaida wanaume wana asili ya ubishi na kupinga
hoja za wengine, sio za wanawake tu hata za wanaume wenzao, hii ni kwasababu ya
kiasili kwamba wanaume ni watu wanaosukumwa na kutaka au kuona ushahidi au
sababu za uthibitisho katika kila kinachosemwa. Kwa bahati mbaya wakiona au
kuhisi tabia hii kwa mwanamke basi ghafla huhamaki na kuhofia kujikita kwenye
mahusiano na mtu wa aina hii wakiogopa kuja kushindana au kukwaruzana huko
baadae.
- Wanapoona au kugundua dalili za kutawaliwa au kukaliwa
Kwa kawaida wanaume wanafuata mapokeo ya asili kwamba
wao ni viongozi na watawala wa familia, wao hutaka kuliona hili hata kabla
hamjaingia kwenye ndoa. Kwa bahati mbaya wako wanawake au kwasababu za kiasili
au malezi na makuzi wamekuwa ni wenye kutaka kupewa nafasi, kutaka kuamrisha,
kuongoza au kufanya maamuzi kwa wengine na wasio rahisi kuongozwa. Wanawake wa
jinsi hii nio rahisi sana kukimbiwa na kila mwanaume anayetaka kuwanao kwenye
mahusiano, au hata kama wameishia kuoana basi hukutana na mashindano au
misuguano mikali kwasababu mwanaume huona ni bora ndoa ife kuliko kuipoteza
nafasi yake ya uongozi au ukuu wa familia hususani katika nguvu ya kufanya
maamuzi. Katika kujitutumua huku mwanaume anaweza kuonyesha tabia nyingi sana
zenye kumuumiza mwanamke, kama vile hasira za mara kwa mara na za ghafla, fujo,
matusi, na visasi vya aina nyingi.
- Wanapoona ukaribu au utegemezi mkubwa wa wazazi au ndugu zako
Ndoa imetengenezwa katika hali ya kwamba wanandoa wote
wanatakiwa kuwaacha wazazi au ndugu zao na kushikamana na wenza wao katika
mambo yote ikiwemo maamuzi yao. Wanaume wengi huwa makini sana tena kimya kimya
kuangalia jinsi wapenzi wao wa kike wanavyohusiana na wazazi wao na ndugu zao
wengine. Iwapo watagundua umemezwa, umekamatwa na kushikwa jumla na nduguzako,
hauwezi kufanya maamuzi yeyote bila wao kuyaridhia, hatayale yamhusuyo mumewako
basi wao huhamaki na kuwa na hofu kubwa huku mioyo yao ikiona kama wao ndio
wameolewa badala ya kuoa. Hisia hizi ni mbaya sana kwa mwanaume, na hivyo
kuweza kujihami kwa kurusha mishale ya maneno na kuamsha misuguano mingine,
sawa sawa na ile niliyoisema kwenye sababu ya nne. Kushirikiana na ndugu zetu
sio kitu kibaya ili mradi nafasi ya mume ibaki pale pale na kuheshimiwa hata
kama mchango wake kiuchumi hauonekani kuwa na mashiko. Kwa upande mwingine
katika hili, inaweza kumuwia ngumu kuolewa binti anayetegemewa kwa asilimia 100
na ndugu au wazazi wake, kwa maana kila kijana anayejileta kwake hata kama
binti ni mzuri, bado kijana anaona mzigo mkubwa mbeleni na kuamua kumwepa au
mumkimbia.
- Wanapogundua ugumu au matatizo fulani kwenye tendo la ndoa
Ni ukweli usiopingika kwamba wanaume wameumbwa kupenda
na kutamani kufanya tendo la ndoa mara kwa mara, wao ni rahisi sana kukimbizwa
katika mahusiano yao na mwanamke pale wanapogundua au kukutana na ugumu wowote
kwenye suala zima la ufanyaji wa tendo la ndoa, ingawa ni mara chache sana
wanaweza kuwa wazi wakwambie nini kinacho wasumbua au wasichokipenda, labda
muwe na kiwango cha juu sana cha mawasiliano. Baadhi ya vitu vinavyoweza kuleta
ugumu au changamoto kwenye tendo la ndoa na kumfanya mwanaume akimbie ni kama
vile, umbo kubwa au uzito wa mpenzi wake wa kike, harufu mbaya ya sehemu za
siri au maeneo mengine ya mwili kama vile chini ya matiti, mdomoni au puani,
changamoto nyingine ni kama vile ukavu uliopitiliza, au uchafu mwingine wa
mwili usiovumilika. Mambo haya na mengine yanayofanana na haya huweza
kumkimbiza mwanaume mapema sana, tena akakimbia kimya kimya na labda baadae
ndiyo unaweza kusikia akilalamika pembeni kuhusu kisa kilichomkimbiza kwako.
- Akigundua unamtoto/watoto au uliwahi kutoa mimba
Wanaume wengi huwa na kiu ya kuja kuanza familia zao
wao wenyewe na sio kukuta mtoto wa mwingine. Ni rahisi sana mwanamke akamkuta
mtoto wa mumewe na akaendelea kuishi naye kuliko mwanaume kumkuta mtoto wa mke wake
na kuishi naye bila matatizo. Hii ndio maana kinadada wengi wakisha pata
ujauzito kabla ya kuolewa wanahisi au wanakumbana na changamoto kubwa sana
katika kuchumbiwa na wanaume wengine kwasababu tu mtoto anakuwa kikwazo.
Vilevile mwanaume anapogundua kama mpenzi wake amewahi kutoa mimba huwa anakuwa
na hofu ya kuendelea na mahusiano maana anakuwa kwenye njia panda ya uhakika wa
kupata mtoto au la. Sio tu kutoa mimba bali hata sababu au mazingira yeyote
yanayoweza kumpa mwanaume hofu au mashaka ya kuja kupata mtoto, haya yanaweza
kumkimbiza mwanaume kutoka kwenye mahusiano mliyonayo, ingawa akianza kuchomoka
huwa anatumia visingizio vingi na sio sababu halisi. Ushauri wangu katika hili
ni kwamba, kama unamtoto basi usifiche, jaribuni kuongea mapema na kuelewana,
kama mtoto ni wa mwanamke au mtoto ni wa mwanaume, yawekeni mezani mapema,
kwamaana yakija kujulikana huko mbeleni huwa yanaleta maumivu makali na visa
visivyoisha na vinavyoendeleza machungu katika ndoa na hata kupelekea ndoa
kuvunjika.
CREDITY >> CHRIS MAUKA
CREDITY >> CHRIS MAUKA