Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, limemuua kwa kumpiga risasi mtu anayedhaniwa kuwa kiongozi wa kundi la watekaji na wauaji wa watu wanao...

Jeshi
la Polisi Mkoa wa Geita, limemuua kwa kumpiga risasi mtu anayedhaniwa
kuwa kiongozi wa kundi la watekaji na wauaji wa watu wanaotekwa kwa
lengo la kujipatia fedha.
Polisi
ilisema jana kuwa mtu huyo aliuawa wakati alipojaribu kuwatoroka punde
baada ya kuonyesha mashimo mawili yaliyokuwa na miili ya watu aliowaua
baada ya kuwateka.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Geita, Kamanda wa
Polisi Mkoa, Mponjoli Lotson alimtaja marehemu huyo kuwa Panda Kinasa.
Alisema aliuawa juzi wilayani Bukombe mkoani Geita kwa kupigwa risasi baada ya kupewa onyo na kukaidi kusimama.
Kamanda
Mpojoli alisema Kinasa alipigwa risasi kwenye tako na alifaraiki dunia
wakati akikimbizwa kwenda Hospitali ya Bukombe, kutokana na kupoteza
damu nyingi.
Mwezi
uliopita katika nyakati tofauti, alisema kamanda huyo, mtuhumiwa
alivamia nyumba ya mfugaji Mbuga Siga katika kijiji cha Ikuzi Lunzewe
wilayani Mbogwe usiku wa saa tatu na kumteka mchunga ng'ombe wake Renard
Samwel mwenye umri wa miaka 18.
Akisimulia
zaidi, Kamanda Mponjoli alisema baada ya kutekeleza utekaji huo,
mtuhumiwa aliacha karatasi yenye ujumbe na namba ya simu 0752 901908
akielekeza kutumiwa Sh. milioni 2 kwenye namba hiyo ili aweze kumuachia
huru mateka.
"Familia
ilitoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada ambapo upelelezi ulianza
kwa kufuatilia namba hiyo kupitia kitengo maalum cha Jeshi la Polisi
kinachohusiana na makosa ya uhalifu wa mitandao ili kubaini alipo
mtuhumiwa," alisema.
Wakati
polisi ikiendelea na upelelezi wa tukio hilo, Mei 7 saa saba za usiku
mtuhumiwa alivamia tena katika kitongoji cha Bwendaseko, Kijiji cha
Buganzu wilayani Bukombe na kumteka Nkwambi Mwandu (25), alisema kamanda
huyo.
Baada
ya utekaji huo pia aliacha ujumbe na namba ile ile 0752 901908
ukielekeza atumiwe Sh. milioni 7 ili aweze kumuachia Nkwambi, alisema.
Kamanda Mponjoli alisema familia ya Nkwambi ilimudu kutuma Sh. 500,000 kwa mpesa na kisha kuripoti Polisi.
Kutokana
na ripoti ya pili hiyo iliilazimu kuendeshwa operesheni maalum ambapo
Mei 31 polisi walifanikiwa kumnasa mtuhumiwa kupitia mtandao na baada ya
kuhojiwa alikiri kuhusika na matukio yote mawili, alisema.
"Baada
ya kumkamata mtuhumiwa alikiri na kuwapeleka makachero wa polisi katika
msitu uliopo Kijiji cha Msasa na kisha kuwaonyesha shimo lenye urefu wa
zaidi ya futi 20 ambamo mwili wa Renard Samwel ulikuwa umetupwa na
kutelekezwa," alisema Kamanda Mponjoli. Mwili huo umetambuliwa na ndugu
zake.
Mtuhumiwa
Kinasa anayedaiwa na polisi kuwa na ujuzi na ubobezi katika matumizi na
kucheza na mtandao wa simu, alidai alimuua Samwel baada ndugu zake
kushindwa kumtumia fedha aliyokuwa ameomba ili aweze kumuachia.
"Baada
ya kuonyesha mwili huo mtuhumiwa aliwapeleka tena (polisi) katika shimo
jingine katika msitu uliopo katika kitongoji cha Ibogolre wilayani
Mbogwe na kuwaonyesha mwili wa marehemu Nkwabi Mwandu uliokuwa umetupwa
na kutelekezwa kwenye shimo lenye urefu wa zaidi ya futi 30," alisema
kamanda huyo na kwamba "nao umetambuliwa na ndugu zake."
Baada
ya kuonyesha miili yote miwili, mtuhumiwa Kinasa alimpinga kikumbo
mmoja wa askari aliokuwa nao na kuanza kukimbia kwa lengo la kutoroka,
alisema zaidi Kamanda Mponjoli na kwamba hata baada ya kupewa onyo la
kusimama, alikaidi na ndipo polisi walipomfyatulia risasi na kumpiga
takoni.
Mwili
wake umehifadhiwa katika Hosptali ya Wilaya ya Bukombe na polisi
inaendelea na upelelezi ili kuwatambua washirika wa mtuhumiwa, alisema.
Credit: Nipashe