Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limesema siku za kumkamata mtuhumiwa wa ujambazi anayeteka watu na kuwapora kwa kutumia bunduki bandia na...

Jeshi
la Polisi mkoani Kigoma limesema siku za kumkamata mtuhumiwa wa
ujambazi anayeteka watu na kuwapora kwa kutumia bunduki bandia na kisu,
zinahesabika.
Limesema kuwa mtuhumiwa huyo amenusurika kukamatwa mara mbili baada ya kuwekewa mtego na polisi.
Akizungumza
leo Alhamisi Mei 24, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin
Ottieno amesema mtuhumiwa huyo ambaye jina lake halisi halijulikani,
anafanya uhalifu kwa kuteka watu na kuwapora mali zao katika barabara ya
Kisili-Buhigwe kwenye pori la Kwitanga.
Pori hilo lipo katikati ya kijiji cha Mahembe na Gereza la Kwitanga katika wilaya ya Kigoma.
"Tunaendelea
kumsaka na polisi wamemkurupusha mara mbili ikabidi adondoshe bunduki
yake chini, kumbe ni ya bandia na ndio anayotumia kupora watu," amesema
Ottieno.
“Bunduki
hizo bandia zimechongwa kwa kutumia mbao kiasi kwamba mtu akiitazama
kwa mbali bila kuichunguza hawezi kutambua kama ni bandia.”
Mtuhumiwa
huyo anadaiwa kupora watu wanaopita barabarani wakiwa kwenye magari,
pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu ambapo hunyang'anya simu za
mkononi na fedha.
Ottieno ameomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano wa dhati kwa askari ili iwe rahisi kumkamata jambazi huyo.



